Paris, Ufaransa
Kocha wa PSG ya Ufaransa, Luis Enrique amesema bado anaamini mshambuliaji Kylian Mbappe anaweza kubadili maamuzi na kubaki timu hiyo licha ya kuhusishwa kwa kiasi kikubwa na mipango ya kujiunga na Real Madrid.
Kauli ya kocha huyo imekuja wakati tayari kuna habari za muda mrefu kwamba mchezaji huyo ameshawaarifu mabosi PSG kwamba hatoongeza mkataba baada ya msimu huu.
Mbappe ametoa kauli hiyo huku habari zaidi zikidai kwamba ameshaweka wazi nia yake ya kutaka kujiunga na klabu ya Real Madrid ambayo imekuwa ikimsaka kwa kipindi kirefu.
Habari zaidi zinadai kwamba Mbappe na Real Madrid wapo katika mazungumzo ingawa hakuna makubaliano yoyote waliyofikia na kusaini licha ya kwamba baada ya msimu huu mkataba wa mchezaji na PSG utafikia mwisho.
Akizungumza jana Jumamosi, Enrique alisema kwamba bado hajakata tamaa kwa mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa kubaki katika jiji la Paris na kuendelea kuichezea PSG.
Enrique aliulizwa kuhusu mechi ya PSG na mahasimu wao Marseille itakayopigwa leo Jumapili na kama ataitumia mechi hiyo kwa kumpanga Mbappe kama derby yake ya mwisho lakini kocha huyo aliwahi kupinga hoja hiyo.
“Kwa nini hii itakuwa derby yake ya mwisho?” alihoji kwa haraka Enrique mara tu baada ya kuulizwa swali hilo.
“Mimi nimeendelea kuwa na matumaini kwamba Kylian atabadili maamuzi, hajasema lolote kwa sasa, anaweza akabadili maamuzi,” alisema Enrique.
“Fikiria tu kama tutashinda mataji manne msimu huu na Kylian Mbappe kuamua katika dakika za mwisho kwamba anataka kubaki Paris, kwa nini isiwe hivyo, ngoja tuone,” alisema Enrique.
Katika mechi za hivi karibuni za PSG, Enrique alikuwa akimuweka benchi Mbappe akidai kwamba wakati wowote timu yake inaweza kumkosa mchezaji huyo hivyo lazima wajiandae kwa hali hiyo.