Na mwandishi wetu
Azam FC imesema inaupa uzito mkubwa mchezo wao wa raundi ya nne ya Kombe la FA (ASFC) dhidi ya Mtibwa Sugar kuhakikisha wanafanya vizuri.
Wanalambalamba hao watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar katika mchezo huo wa Aprili 7, mwaka huu kwenye, Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam huku wakiahidi kutoichukulia poa timu ya Mtibwa.
Akiizungumzia mechi hiyo ofisa habari wa Azam, Thabit Zakaria amesema watu wanaichukulia poa Mtibwa kwa sababu haifanyi vizuri lakini wao wanaitazama tofauti na watakwenda kwa tahadhari zote kwenye mchezo huo.
“Unaweza kuiona Mtibwa ni timu dhaifu lakini wakikufunga itakuwa aibu, lazima tujiandae vizuri ili watu wasije na hoja kuwa tumefungwa na timu inayoshika mkia kwenye ligi, hatutaki hilo litokee, sisi tunawaheshimu na kujipanga dhidi yao,” alisema Zakaria.
Zakaria aliongeza kuwa kuelekea maandalizi ya mchezo huo wachezaji wote wako vizuri isipokuwa kwa baadhi ya wachezaji waliokuwa majeruhi ambao wameanza mazoezi mepesi.
Aliwataja wachezaji hao kuwa ni Sospeter Bajana, Franklin Navaro na Abdallah Kheri ambao wanajiandaa na mechi za usoni.