Berlin, Ujerumani
Kocha wa Bayer Leverkusen, Xabi Alonso ambaye amekuwa akihusishwa mpango wa kujiunga na Liverpool hatimaye amevunja ukimya akisema hana mpango wa kuondoka Leverkusen kwa sasa.
Alonso amekuwa akiifurahia kazi yake katika timu hiyo ambayo inaelekea kutwaa taji la Ligi Kuu Ujerumani au Bundesliga ikiwa haijapoteza hata mchezo mmoja msimu huu katika mashindano yote.
Akifafanua kuhusu uamuzi wake wa kubaki katika timu hiyo, Alonso alisema kwamba Leverkusen ni sehemu sahihi kwa kocha ‘mchanga’ kama yeye kama klabu yenyewe ilivyo ‘changa’.
Tangu kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp atangaze kuwa ataachana na timu hiyo baada ya msimu huu, jina la Alonso limechomoza na kuwa namba moja akihusishwa kumrithi Klopp.
Alonso, 42, kiungo wa zamani wa Liverpool mbali na kuhusishwa na timu yake hiyo ya zamani pia amekuwa akitajwa katika klabu kigogo ya Ujerumani ya Bayern Munich.
Bayern kwa sasa inasaka kocha mpya baada ya kufikia makubaliano ya kuachana na kocha wake wa sasa, Thomas Tuchel atakayeondoka baada ya msimu huu na Alonso pia amekuwa akitajwa kuwa mtu sahihi kumrithi Tuchel.
Wiki iliyopita Alonso aliwaarifu wakurugenzi wa Leverkusen kuhusu uamuzi wake wa kuendelea kuwa kocha wa timu hiyo akisema kwamba huo ni uamuzi sahihi.
“Naamini ni uamuzi sahihi na nina furaha, tumekuwa na uvumi mwingi kuhusu mambo yangu yajayo, hadi sasa tumekuwa na mechi nyingi na niko makini katika hilo na nilitaka kutafakari wakati wa mapumziko ya mechi za kimataifa na kuchukua uamuzi,” alisema Alonso.
“Wachezaji wamenipa sababu nyingi za kuiamini timu, kujituma kwao, shauku, njaa ya kuwa na msimu bora, kazi yangu bado haijaisha hapa,” alisema Alonso.
Akiwa mchezaji Liverpool, Alonso aliweka rekodi ya kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2005 ingawa aliihama mwaka 2009 na kujinga na Real Madrid, klabu nyingine ambayo pia inadaiwa kuonesha nia ya kumtaka awe kocha wao baada ya Carlo Ancelotti.
Baada ya Real Madrid, Alonso alijiunga na Bayern miaka mitano baadaye kabla ya kustaafu soka la ushindani mwaka 2017 na hatimaye kujikita katika kazi ya ukocha mwaka 2018 akianzia kwenye timu ya vijana chini ya miaka 14 ya Real Madrid.