Madrid, Hispania
Waendesha mashtaka wa Mahakama Kuu Hispania wamewasilisha hoja ya kutaka rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Hispania, Luis Rubiales afungwe jela miaka miwili na nusu kwa kosa la kumbusu mdomoni mchezaji wa timu ya taifa ya Hispania, Jenni Hermoso.
Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha habari, waendesha mashtaka hao wanamshitaki Rubiales kwa kosa moja la udhalilishaji kijinsia na kocha jingine la kutumia ubabe baada ya tukio la kumbusu Jenni.
Madai ya ofisi ya waendesha mashtaka ni kwamba makosa hayo mawili kila moja lina adhabu yake, la kwanza ni kifungo cha mwaka mmoja jela na la pili ni kifungo cha mwaka mmoja na nusu jela na hivyo wanataka Rubiales aadhibiwe kwa makosa yote hayo mawili.
Rubiales, 46, (pichani chini), alimbusu Jenni Agosti 20 mwaka jana mara baada ya Hispania kuibwaga England katika mechi ya fainali ya Kombe la Dunia la Wanawake na kubeba taji hilo mjini Sydney, Australia.
Wakati wachezaji wakivalishwa medali za ushindi, Rubiales akionekana kama mtu aliyepagawa na ushindi huo, alimkumbatia Jenni kwa nguvu na kumpiga busu la mdomoni hali iliyozua taharuki.

Waendesha mashtaka hao pia mbali na Rubiales wanawashaki aliyekuwa kocha timu ya wanawake ya HIspania, Jorge Vilda, mkurugenzi wa michezo wa timu hiyo, Albert Luque na mkuu wa masoko wa shirikisho, Ruben Rivera kwa kumshinikiza Jenni aseme kwamba kulikuwa na makubaliano kati yake na Rubiales kabla ya kupigwa busu.
Pia wanataka Rubiales peke yake alipe faini ya Dola 54,000 kama fidia kwa Jenni wakati Vilda, Luque, Rivera na Rubiales tena kwa pamoja walipe kiasi kama hicho cha fedha.
Awali Rubiales alisema kwamba kulikuwa na makubaliano kati yake na Jenni hadi akampiga busu na kukataa kujiuzulu licha ya kushutumiwa na kushinikizwa na watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa serikali ajiuzulu nafasi aliyokuwa akiishikilia ya urais wa Shirikisho la Soka Hispania.
Baadaye Fifa iliingilia kati suala hilo na kumsimamisha Rubiales kwa miezi mitatu ili kupisha uchunguzi wa tukio hilo ingawa baadaye mwenyewe alitangaza kujiuzulu.