Beijing, China
Rais wa zamani wa Chama cha Soka China (CFA), Chen Xuyuan (pichani) amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kujihusisha na rushwa.
Taarifa za vyanzo vya habari nchini China zinaeleza kuwa Januari mwaka huu kiongozi huyo alikiri kuchukua pesa zinazodaiwa kuwa ni zao la rushwa na ufisadi zinazofikia Dola 11.8 milioni.
Hatua ya kiongozi huyo kukamatwa na kushitakiwa imekuja baada ya rais wa China, Xi Jinping kuanzisha kampeni ya kupambana na ufisadi ambayo imeangazia sekta ya michezo, benki na jeshi.
Katika soka habari zinadai kwamba makocha na wachezaji kadhaa wanaendelea kuhojiwa na kuchunguzwa kuhusiana na matukio ya rushwa.
Kuhusu Xuyuan, taarifa za kimahakama zilieleza kuwa kiongozi huyo anadaiwa kujihusisha na ufisadi kati ya mwaka 2010 hadi 2023 ambapo katika kipindi hicho mbali na urais wa CFA pia alikuwa mwenyekiti wa Shanghai International Port Group.
Waendesha mashitaka walidai kuwa Xuyuan alipokea fedha na vitu mbalimbali kwa makubaliano ya kusaidia upatikanaji wa miradi ya ujenzi na kuandaa matukio ya kimichezo.
Mbali na Xuyuan, viongozi wengine waandamizi watatu wa kwenye soka nao walihukumiwa kifungo cha jela kati ya miaka minane hadi 14 kwa makosa tofauti tofauti ya rushwa na ufisadi.
Mapema mwaka huu kiungo wa zamani wa Everton ambaye pia amewahi kuwa kocha wa timu ya taifa ya soka ya China, Lie Tie alikiri kupanga matokeo ya mechi kadhaa na kutoa rushwa kwa baadhi ya watu akiwamo Chen ili apate kazi ya ukocha katika timu ya taifa ya China.
Mwaka 2011 Rais Jinping alinukuliwa akisema kwamba anataka kuifanya China iwe taifa kubwa katika soka na katika hali alitaka kufanikisha mambo matatu ambayo ni kufuzu Kombe la Dunia, kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia na kubeba Kombe la Dunia.
Katika tukio jingine taarifa za Wizara ya Mambo ya Nje zilieleza kuwa mchezaji nyota wa Korea Kusini, Son Jun-ho anayeichezea Shandong Taishan alikamatwa na polisi na kuwekwa kizuizini kwa tuhuma za rushwa lakini baadaye aliachiwa huru.
Kimataifa Bosi wa soka China jela maisha kwa rushwa
Bosi wa soka China jela maisha kwa rushwa
Read also