Na mwandishi wetu
Baada ya kupoteza mchezo wa Fifa Series 2024 kwa bao 1-0 dhidi ya Bulgaria, kaimu kocha mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ amesema amefurahishwa na kiwango cha upambanaji kilichooneshwa na wachezaji wake.
Stars ilipoteza mechi hiyo ya kwanza iliyopigwa Ijumaa kwenye Uwanja wa Uwanja wa Dalga, Azerbaijan lakini kocha Morocco ameona faraja kwa kuongezeka hali ya upambanaji ndani ya kikosi na wao kama benchi la ufundi watajitahidi kukazia hapo ili kufanya wachezaji waimarike zaidi.
“Si rahisi kuwa na muendelezo ule kwa dakika 90 kutokana na presha iliyokuwepo, mpira uko hivyo kuna muda unamiliki na wakati mwingine unapoteza umiliki wa mchezo, tutaweza kufanya vizuri zaidi kama tukipata muda.
“Lakini hata hali ya hewa pia inaweza kuwa chanzo ila maadamu tulikuwa tunapata nafasi ya kujaribu kwa kuisukuma timu mbele ilikuwa inaonekana kuna kitu tunaweza kufanya,” alisema Morocco.
.
Alisema vjana wake waliweza kumiliki mpira hiyo ndio falsafa yake anaamini kama ukimiliki mpira na kutengeneza nafasi una nafasi ya kufunga.
Naye nahodha wa mchezo huo, Himid Mao alisema: “Mechi ilikuwa imegawanyika asilimia 50 kwa 50, wao walikuwa na nafasi na sisi tulikuwa na nafasi, katika nafasi walizopata moja wakaitumia ila matokeo yalikuwa sawa kabisa.
“Naamini sisi kama wachezaji na benchi zima la ufundi wameona nini kilikosekana pale, tutaenda kwenye uwanja wa mazoezi kurekebisha kwa ajili ya michezo inayokuja.”