Paris, Ufaransa
Kiungo wa timu ya vijana chini ya miaka 19 ya Ufaransa, Mahamadou Diawara inadaiwa kaondoka katika kikosi cha timu hiyo kutokana na sheria inayopiga marufuku mchezaji kuwa kwenye timu ya taifa akiwa amefunga.
Habari za ndani zinadai kuwa Diawarra amechukua uamuzi huo kutokana na sheria ya Shirikisho la Soka Ufaransa (FFF) kupiga marufuku wachezaji walio kwenye timu ya taifa kufunga katika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhan.
Inadaiwa sheria hiyo inatumika kuanzia kwa wachezaji wa umri chini ya miaka 16 hadi wa kikosi cha wakubwa jambo ambalo halikumfurahisha Diawara na hatimaye akaamua kurudi kwenye kikosi cha timu yake ya Lyon.
Taarifa ya FFF ilithibitisha Diawara kuondoka katika kikosi cha timu ya taifa na tayari Dehmaine Tabibou wa Nantes ameitwa kuziba pengo la mchezaji huyo.
Rais wa FFF, Philippe Diallo aliwahi kusema katika mahojiano aliyofanya na gazeti moja la Ufaransa kwamba ameweka sheria zinazowahusu wachezaji walio kwenye timu ya taifa kuhusu kufunga katika kipindi cha mwezi wa Ramadhan.
Diallo alisema kwamba kuna kanuni ya kwenye shirikisho hilo yenye kuepusha muingiliano ili kuhakikisha kwamba mambo ya dini hayaingiliani na mambo ya mwanamichezo.
Sheria hiyo ya FFF inaeleza kuwa mchezaji anapoitwa katika timu mojawapo ya taifa ya Ufaransa hatoweza kufunga mfungo wa Ramadhan badala yake wachezaji watatakiwa kufuata kanuni za timu, mshikamano na majukumu mengine.
Sheria hiyo imeonekana kuwakera baadhi ya wachezaji ambao baadhi yao wanajiona kama hawapewi heshima wao pamoja na dini yao.
Baadhi ya wachezaji inadaiwa wameamua kukaa kimya kwa kutotaka kusababisha mvutano lakini kwa Diawara hali imekuwa tofauti, hakufurahia jambo hilo, akaamua bora aondoke kwenye timu hiyo.
Kimataifa Ajitoa timu ya taifa Ufaransa kwa kuzuiwa kufunga Ramadhan
Ajitoa timu ya taifa Ufaransa kwa kuzuiwa kufunga Ramadhan
Related posts
Read also