Rio de Janeiro, Brazil
Hatimaye Mahakama Kuu Brazil imeamua nyota wa zamani wa AC Milan, Real Madrid na Man City, Robinho lazima atumikie adhabu ya kifungo cha miaka tisa jela kwa kosa la kubaka alilolifanya akiwa Italia.
Robinho anadaiwa kufanya kosa hilo mwaka 2013 wakati huo akiwa mchezaji wa AC Milan na kuhukumiwa na makahama ya Italia kifungo cha miaka tisa jela lakini alikuwa tayari amerudi kwao Brazil.
Mchezaji huyo ambaye pia amewahi kutamba na timu ya taifa ya Brazil anadaiwa pamoja na kundi la vijana wenzake walimbaka msichana mmoja na mahakama Italia kuomba atumikie adhabu hiyo akiwa Brazil.
Kwa mantiki hiyo uamuzi wa Mahakama Kuu Brazil unakazia hukumu ya awali aliyopewa mchezaji huyo nchini Italia kwa kuwa sheria za Brazil hazina utaratibu wa kuwapeleka watuhumiwa kwenda kutumikia adhabu katika nchi ambayo walifanya kosa husika.
Majaji 15 waliosikiliza shauri hilo walipiga kura ambapo kati yao tisa walipitisha uamuzi wa Robinho kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka tisa jela wakati ni wawili tu ambao waliukataa.
Katika hoja yake ya kutaka Robinho ahukumiwe nchini Brazil, jaji mmoja alisema kwamba mchezaji huyo hawezi kuachwa bila ya kutumikia adhabu kufanya hivyo kunaweza kusababisha mgogoro wa kidiplomasia kati ya Italia na Brazil.
Naye wakili wa msichana anayedaiwa kubakwa, alisema yeye na mteja wake wameridhishwa na uamuzi wa Mahakama Kuu Brazil na wanaheshimu na kuelewa kuwa sheria za Brazil haziruhusu mshitakiwa kupelekwa kutumikia adhabu katika nchi aliyofanya kosa husika.
Wakili wa Robinho hata hivyo alisema ataukatia rufaa uamuzi huo katika mahakama ya juu zaidi na kutaka mchezaji huyo asikamatwe badala yake aendelee kuwa huru wakati wote wa kusikilizwa kwa rufaa hiyo.
Robinho, 40, ambaye kwa sasa anaishi Santos, alishakabidhi hati yake ya kusafiria kwa mamlaka husika nchini Brazil tangu Machi 2023 na ameendelea kukana kufanya kosa lolote.
Mchezaji huyo ambaye pia amewahi kuichezea klabu ya Santos ya Brazil alisema kwamba kulikuwa na makubaliano kati yake na msichana husika kabla ya tukio hilo analodaiwa kulifanya akishirikiana na wenzake kwenye baa moja ya mjini Milan.