Manchester, England
Bilionea na mmiliki mwenza wa Manchester United, Sir Jim Ratcliffe amefuta hesabu zozote za kumsajili mshambuliaji wa PSG, Kylian Mbappe badala yake anataka klabu hiyo imsajili ‘Mbappe ajaye’.
Ratcliffe na jopo lake wakiongozwa na Sir Dave Brailsford wanajiandaa kufanya usajili wa nguvu katika majira ya kiangazi ambao utakuwa ni usajili wa kwanza kwa bilionea huyo tangu anunue hisa asilimia 27.7 katika klabu hiyo.
Mbappe katika kipindi cha majira ya kiangazi msimu huu atakuwa huru baada ya kumaliza mkataba wake na PSG na tayari ametangaza kuihama timu hiyo huku akihusishwa zaidi na mpango wa kujiunga na Real Madrid.
Ukiacha Real Madrid, Mbappe pia amewahi kuhusishwa na klabu za Liverpool, Arsenal na sasa Man United lakini Ratcliffe amefuta rasmi mpango huo akisema kwamba anadhani watakachoangalia ni kusajili vipaji vinavyoibukia badala ya mastaa ambao tayari wana majina.
“Nafikiri katika hilo jambo ambalo naona ni bora kulifanya ni kujaribu kumsajili Mbappe ajaye badala ya kutumia rasilimali kununua mafanikio,” alisema Ratcliffe.
“Si jambo la busara kumnunua Mbappe, kila mmoja anaweza kulifanyia tafakuri jambo hilo, changamoto kubwa zaidi ni kumtafuta Mbappe ajaye au Jude Bellingham au Roy Keane,” alisema Ratcliffe.
Bilionea huyo alifafanua kuwa suluhisho si kutumia fedha nyingi kwa kununua wachezaji wakubwa kwani jambo hilo limeshafanyika ukiangalia kipindi cha miaka 10 iliyopita namna fedha zilivyotumika kusajili wachezaji wakubwa.
“Jambo la kwanza unalotakiwa kufanya ni kuwa na watu sahi katika eneo sahihi la kuongoza klabu na kuhakikisha kuna utaratibu sahihi wa kukuza vipaji, hilo ni eneo muhimu katika klabu ya soka, kukuzavipaji kwa namna sahihi,” alisema Ratcliffe.
Ratcliffe (pichani) tayari ameanza kufanya mabadiliko kadhaa katika klabu hiyo, amemuajiri Omar Berrada kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) mpya akitokea Man City pamoja na Dan Ashworth kutoka Newcastle United ambaye anakuwa mkurugenzi mpya wa michezo.
Swali lililobaki ni kuhusu nafasi ya kocha Erik ten Hag kama ataendelea naye au atamuacha ingawa bilionea huyo anatajwa kuvutiwa na utendaji wa Jurgen Klopp wa Liverpool ambaye ameshatangaza kuachana na timu hiyo baada ya msimu huu.