Na mwandishi wetu
Nahodha wa timu ya KMC, Awesu Awesu amesema watapambana kuhakikisha wanashinda mechi zao tisa zilizobaki ili kumaliza msimu ndani ya nafasi nne za juu kwenye Ligi Kuu NBC.
Alisema kwamba kwa kufanya hivyo watakuwa wamewazidi kete Coastal Union waliowazidi kwa pointi mbili na Tanzania Prisons waliofungana nao kwa pointi.
Awesu ambaye yupo kwenye kiwango bora kwa sasa alisema lengo lao kubwa ni kushiriki michuano ya kimataifa kama walivyowahi kufanya katika misimu mitatu nyuma.
“Tumekuwa na msimu bora sana, itapendeza kama tutamaliza ndani ya nne bora ingawa najua vita ni kali lakini tutapambana kwa ajili ya kutimiza lengo letu,” alisema Awesu.
Kiungo huyo ambaye pia anaichezea timu ya taifa ya Zanzibar, ‘Zanzibar Heroes’ alisema mbali na kutaka kushiriki mashindano ya kimataifa msimu ujao lakini anaamini timu hiyo itafanya usajili mkubwa zaidi ili msimu ujao wawe miongoni mwa timu zinazowania ubingwa wa ligi kuu.
Alisema anajivunia ubora wa kikosi chao pamoja na uwezo mkubwa alionao chini ya kocha wao, Abdulhamid Moallin ambaye anaonekana kuibadili timu hiyo kwa kiasi kikubwa.
KMC inashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 28 sawa na Prisons inayoshika nafasi ya tano huku Coastal iking’ang’ania nafasi ya nne kwa pointi zake 30 baada ya kila timu kushuka dimbani mara 21.
Soka Awesu ataka ushindi mechi zilizobaki
Awesu ataka ushindi mechi zilizobaki
Read also