Na mwandishi wetu
Kaimu kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Hemed Morocco amesema wana wakati mgumu juu ya hali ya hewa ya baridi kali nchini Azerbaijan walikokwenda kushiriki michezo ya kirafiki ya Fifa Series.
Stars ni miongoni mwa timu 24 zitakazoshiriki mashindano hayo maalumu ya kirafiki yaliyoandaliwa katika mataifa matano tofauti.
Mataifa mengine yaliyoandaa mashindano kama hayo ni Algeria, Misri, Saudi Arabia na Sri Lanka na yataanza rasmi kesho Alhamisi hadi Machi 26, mwaka huu na Tanzania itafungua dimba dhidi ya Bulgaria.
Akizungumza na GreenSports kuhusiana na timu hiyo iliyotua Azerbaijan jana, Morocco alisema:
“Tunamshukuru Mungu tumefika salama, tumeanza mazoezi na tuko vizuri. Hali ya hewa ni ngumu kwa wachezaji ambao wanatoka Tanzania kwani kuna baridi. Lakini wameanza kuzoea naamini kadiri tunavyokwenda mbele watakuwa vizuri,” alisema Morocco.
Stars baada ya kumalizana na Bulgaria, itavaana na Mongolia Machi 25 katika michuano hiyo iliyopitishwa rasmi na Rais wa Fifa, Gianni Infantino Machi, mwaka jana kwenye kongamano la 73 la Fifa.
Kongamano hilo lilifanyika nchini Rwanda likilenga kuzikutanisha timu kutoka mashirikisho tofauti kujifunza kimbinu, kiufundi na kuangalia fursa nyingine za kimaendeleo na kiuchumi.