Na mwandishi wetu
Ofisa Habari wa Simba SC, Ahmed Ally ameweka wazi sababu ya timu hiyo kufanya mazoezi usiku kuwa ni pendekezo la kocha wao mkuu Abdelhak Benchikha anayetaka kikosi chake kizoee mazingira ya mchezo ili yasiwape shida watakaposhuka kuikabili Al Ahly, Machi 29, mwaka huu.
Akizungumza leo Alhamisi Dar es Salaam, Ahmed alisema watakuwa na kambi ya siku nane na dhumuni la kwenda Zanzibar ni Benchikha kuhitaji utulivu wa hali ya juu kutokana na uzito wa mchezo huo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ulio mbele yao.
“Wengi walitaka mechi ipigwe saa 10 jioni lakini mechi hizi zinapangwa na watu wengi kwa maslahi ya wengi wakiwemo wenye haki za matangazo na CAF wanaangalia mustakabali wa timu zote mbili lakini maslahi mapana ya watu wa imani zote yamezingatiwa na ndio maana ikapangwa saa 3 usiku.
“Niwakumbushe tu Wanasimba hii si mara ya kwanza kucheza mechi usiku, tulicheza dhidi ya USGN muda wa saa 4 usiku na tukamfunga kwa maandalizi tunayofanya InshaAllah tunakwenda kupata matokeo,” alisema Ally.
Alisema Simba ya makundi si itakayocheza robo fainali, itakuwa mpya ambayo inaitaka nusu fainali na hiyo ndio itakuwa mechi bora ya hatua ya robo fainali sababu inamkutanisha bingwa mtetezi na timu namba tano kwa ubora Afrika.
“Tarehe 29 ni siku ya kufa na kupona, siku ya kupambania Simba yetu, tujitahidi kila Mwanasimba aje Uwanja wa Mkapa, mechi yetu ni saa 3 usiku hivyo una chaguo ufuturu nyumbani au uje Uwanja wa Mkapa utafuturu maana futari itakuwepo,” alisema