Madrid, Hispania
Klabu ya Real Madrid imewasilisha malalamiko yake Shirikisho la Soka Hispania dhidi ya ilichokiita uzembe wa mwamuzi wa mechi yao na Osasuna kutoiweka katika ripoti yake kadhia ya ubaguzi wa rangi aliyofanyiwa mchezaji wao Vinicius Junior.
Real Madrid Jumamosi iliyopita iliumana na Osasuna katika Ligi Kuu Hispania au La Liga na kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 lakini katika mechi hiyo Vinicius Jr alidhihakiwa na baadhi ya mashabiki.
Vinicius Jr katika mechi hiyo aliifungia Real Madrid mabao mawili na katika kushangilia bao la pili aliwageukia mashabiki na kuonekana akiweka mkono kwenye sikio ambapo baadaye picha za kwenye televisheni ziliwaonesha baadhi ya mashabiki wakiimba ‘Vinicius afe’.
Mwamuzi wa mechi hiyo, Martinez Munuera, ripoti yake hata hivyo haikujumuisha matukio hayo jambo ambalo limewakera mabosi wa Real Madrid na kuamua kuchukua hatua.
“Baada ya dhihaka kubwa kufanywa kwa mara nyingine dhidi ya mchezaji wetu Vinicius Junior, katika tukio la mwisho la mechi yetu ya La Liga, Real Madrid inapenda kusema yafuatayo…
“Klabu yetu imewasilisha malalamiko kwenye Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho dhidi ya mwamuzi wa mechi Martinez Munuera kutokana na uzembe wa kwenye ripoti ya mwamuzi.
“Mwamuzi kwa makusudi kabisa aliondoa udhalilishaji huo na kauli za kuudhi zilizokuwa zikirudiwa kwa mchezaji wetu Vinicius Junior, licha ya kuonywa mara kadhaa na wachezaji wetu mara baada ya matukio hayo kujitokeza,” ilieleza taarifa ya klabu hiyo.
Mara kadhaa Vinicius Jr amejikuta akiwa mlengwa wa kadhia za ubaguzi wa rangi kutoka kwa mashabiki wa timu pinzani likiwamo tukio la Mei mwaka jana kwenye Uwanja wa Mestalla katika mechi dhidi ya Valencia na tayari uchunguzi umeanzishwa ukiwahusisha watuhumiwa watatu.