Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema ugumu wa ratiba ni chanzo cha kikosi chake kupoteza mchezo wa Ligi Kuu NBC dhidi ya Azam FC kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Huu unakuwa mchezo wa pili kwa Yanga kupoteza msimu huu baada ya kufungwa 2-1 na Ihefu ingawa Wananchi wameendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa ligi kwa pointi 52 baada ya mechi 21, ikifuatiwa na Azam tenye pointi 47.
“Nina furaha lakini sijui kama nitaeleweka, niombe radhi kuna vitu nikiongea vitaleta picha nzuri, tulianza vizuri mchezo lakini kila mtu ameona kilichofanywa na mwamuzi alipokubali bao la kuotea,” alisema Gamondi kuhusu mechi hiyo iliyopigwa Jumapili iliyopita.
Alisema kitendo cha kucheza michezo mfululizo ya ligi kimeiathiri timu yake ingawa kama ataongea ataonekana kama anatafuta sababu ya kujitetea lakini sio sahihi kucheza mechi nne kwa siku 17.
“Hapa siongelei kuhusu Yanga pekee bali hata Simba kwa kucheza michezo nyumbani na kusafiri ugenini sio jambo rahisi hata kidogo, tumejitahidi sana kupambana,” alisema Gamondi.
“Ukichukua mambo yote haya ukaongeza muda na waamuzi ni chanzo cha kutokuwa bora, mwamuzi wa pembeni aliruhusu bao la kuotea lililowanufaisha wapinzani wetu,” alisema Gamondi
.
Yanga baada kupoteza mbele ya Al Ahly, Machi Mosi, ikaifuata Namungo, Uwanja wa Majaliwa Machi 8 na kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, kisha ikashinda 5-0 dhidi ya Ihefu Machi 11, Uwanja wa Azam Complex kabla ya kuichapa Geita Gold 1-0 Machi 14 na Jumapili ikaumana na Azam.