Na mwandishi wetu
Feisal Salum au Fei Toto ameidhihirishia timu yake ya zamani ya Yanga kwamba bado yuko vizuri baada ya kuifungia Azam FC bao la pili lililoipa timu hiyo ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Yanga.
Fei ataendelea kufurahia ushindi huo hasa akikumbuka jinsi alivyojikuta katika mgogoro na uongozi wa Yanga kutokana na uamuzi wake wa kuvunja mkataba na timu hiyo uliomfanya awe nje ya uwanja kwa kipindi kirefu.
Mgogoro huo hata hivyo ulifikia mwisho baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwaomba viongozi wa Yanga kulimaliza suala hilo na hatimaye mchezaji huyo kuruhusiwa kujiunga na Azam.
Yanga kwa matokeo ya mechi hiyo ya Ligi Kuu NBC iliyopigwa Jumapili hii usiku yanaifanya timu hiyo iwe na unyonge wa kufungwa na Fei Toto lakini pia kupunguzwa kasi yake ya ushindi kwenye ligi hiyo msimu huu.
Yanga ambayo imekuwa ikiinyanyasa Azam katika mechi zao za hivi karibuni pamoja na timu nyingine za ligi hiyo msimu huu, hata hivyo inaendelea kubaki kileleni ikiwa na pointi zake 52.
Kwa upande wa Azam inakuwa imerudi katika nafasi yake ya pili ikiwa na pointi 47 na kuizidi Simba kwa tofauti ya pointi mbili ingawa Azam imecheza michezo 21 ikiwa ni michezo miwili zaidi ya ile ya Simba.
Yanga ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Clement Mzize katika dakika ya 10 lakini ikawachukua Azam dakika tisa kusawazisha kupitia kwa Gibril Sillah na kuzifanya timu hizo ziende mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.
Dakika sita baada ya kuanza kipindi cha pili, Azam walifanya shambulizi kali langoni mwa Yanga na Fei Toto kuuwahi mpira kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa wa Yanga Djigui Diarra.
Yanga katika mechi hiyo ilipata pigo katika kipindi cha kwanza baada ya kiungo wake, Pacome Zouazoua kuumia na nafasi yake kuingia Joseph Guede.
Soka Fei Toto aizamisha Yanga
Fei Toto aizamisha Yanga
Read also