Na mwandishi wetu
Simba imefanikiwa kuiengua Azam FC katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC baada ya kuichapa Mashujaa FC mabao 2-0 katika mechi iliyopigwa Ijumaa hii kwenye dimba la Azam Complex, Dar es Salaam.
Ikionekana imetimia, Simba ilipata tabu kuipenya safu ya ulinzi ya Mashujaa na hadi dakika 45 zinakamilika timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa hazijafungana bao hata moja licha ya kushambuliana mara kadhaa.
Kipindi cha pili, Mashujaa waliendelea kukomaa na kuibua hali ya wasiwasi kwamba huenda wangeifanyia Simba kile walichoifanyia mwaka 2021 kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho Azam (FA) walipoichapa mabao 3-1 na kuitoa katika mashindano hayo.
Matarajio hayo hata hivyo yalianza kufutika katika dakika ya 57 baada ya Clatous Chota Chama kwa mara nyingine kudhihirisha ubora wake kwa kuifungia Simba bao la kwanza na kumalizia la pili dakika ya 73.
Ushindi huo umeifanya Simba kufikisha jumla ya pointi 45 katika mechi 19 na kuishusha Azam hadi nafasi ya tatu ikiwa na ponti 44 katika mechi 20.
Azam hata hivyo inaweza kurudi katika nafasi ya pili kama itaweza kutoka na ushindi katika mechi yao ngumu ya Jumapili dhidi ya Yanga itakayopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Soka Simba yaipiga Mashujaa 2-0
Simba yaipiga Mashujaa 2-0
Read also