Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa timu ya Azam FC, Allasane Diao (pichani kushoto) anatarajia kuzikosa mechi zote za Ligi Kuu NBC zilizosalia za msimu huu baada ya kufanyiwa upasuaji mkubwa wa goti nchini Afrika Kusini.
Diao mwenye mabao matatu mpaka sasa, atakosa mechi 10 za ligi dhidi ya Yanga, Namungo, Mashujaa, Ihefu, Mtibwa Sugar, KMC, Simba, JKT Tanzania, Kagera Sugar na Geita Gold.
Ofisa Habari wa Azam, Thabiti Zacharia alisema Alhamisi hii kuwa Diao amefanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Vincent Palloti ya Cape Town na atakuwa nje kwa kipindi cha miezi saba hadi tisa kuuguza majeraha hayo.
“Tunatarajia kuikosa huduma ya Diao kwa mechi zote za msimu huu zilizosalia baada ya kufanyiwa upasuaji utakaomfanya akae nje kwa muda mrefu.
“Tunashukuru upasuaji ulifanyika kwa mafanikio makubwa, ni pigo kwenye mipango yetu msimu huu lakini tunaamini mwalimu atatumia wachezaji waliopo kuziba pengo lake,” alisema Zacharia.
Wachezaji wengine wa Azam wanaosumbuliwa na majeraha ni Franklin Navaro, Sospeter Bajana, Malickou Ndoye, Ali Ahmada na Abdulai Idrisu.