Na mwandishi wetu
Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mudathir Yahya ameibuka mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Februari ndani ya klabu hiyo akiwazidi Pacome Zouzoua na Nickson Kibabage.
Akizungumza na GreenSports Mudathir aliye kwenye kiwango cha juu kwa sasa, aliwashukuru mashabiki wa timu hiyo kwa kumpigia kura ambazo zimemfanya aibuke mshindi kwenye kinyang’anyiro hicho.
“Nawashukuru mashabiki na wanachama wa Yanga kwa kunipigia kura, kwangu ni kama kuniongezea ari ya kupambana nifanye vizuri zaidi ya hapa, nawashukuru sana,” alisema Mudathir.
Kiungo huyo pia aliwashukuru wachezaji wenzake na wadhamini wa tuzo hizo Shirika la Bima la Taifa (NIC) kwa mchango na mawazo yao ambayo kwa kiasi kikubwa yameongeza hamasa kwa wachezaji.
Kwa kushinda tuzo hiyo, Mudathir ambaye anakuwa mchezaji wa tano kubeba tuzo hiyo tangu ianzishwe Oktoba, mwaka jana, atazawadiwa kitita cha Sh milioni 4 pamoja na kombe dogo kutoka kwa wadhamini hao.