Na mwandishi wetu
Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta na Dickson Job wameachwa katika kikosi kilichoitwa kushiriki michuano ya Fifa Series 2024 itakayofanyika nchini Azerbaijan.
Kikosi hicho cha wachezaji 23 kimetangazwa leo Jumatano na kaimu kocha mkuu wa Stars, Hemed Morocco kuelekea michuano hiyo mipya ya kirafiki ya mwaliko inayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Wachezaji walioitwa kuiwakilisha nchi katika michuano hiyo itakayokuwa ikifanyika mwezi Machi wa kila mwaka ni makipa Aishi Manula wa Simba, Aboutwalib Mshery (Yanga) na Kwesi Kawawa (Syrianska FC, Sweden).
Mabeki ni Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Hamad (wote Yanga), Kennedy Juma, Mohamed Hussein (wote Simba), Lusajo Mwaikenda (Azam), Miano Danilo (Villenna, Hispania), Haji Mnoga (Aldershot, England) na Novatus Dismas (Shaktar Donetsk, Ukraine).
Safu ya kiungo ni Tarryn Allarakhia (Wealdstone, England), Morice Michael (RFK Novi Sad, Serbia), Himid Mao (El Gaish, Misri), Mudathir Yahya (Yanga) Yahya Zaydi na Feisal Salum (wote Azam).
Washambuliaji ni Clement Mzize (Yanga), Kibu Denis (Simba), Abdul Suleiman (Azam), Simon Msuva (Alnajmah, Saudi Arabia), Ben Starkie (Ilkeston Town, England) na Charles M’mombwa (Macarthur FC, Australia).
Michuano hiyo itazileta pamoja timu za taifa za wanaume katika mfululizo wa michuano midogo inayohusisha timu za kutoka mashirikisho ya soka ya mabara sita yanayosimamiwa na Fifa.
Kila kundi litakuwa na timu nne na michuano itafanyika katika kituo kimoja ikitumia muda wa mapumziko ya ligi ya kupisha mechi za kimataifa.
Kimataifa Morocco awaacha Samatta, Job Stars
Morocco awaacha Samatta, Job Stars
Read also