Liverpool, England
Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp amesema timu yake imenyimwa penalti ya wazi kwa asilimia 100 katika mechi yao na Man City iliyoisha kwa sare ya bao 1-1 na kuhoji chakula alichokula mchana msimamizi wa VAR.
Klopp ametoa kauli hiyo kuhusu mechi hiyo iliyopigwa jana Jumapili akihusisha rafu ya dakika za nyongeza aliyochezewa Alexis Mac Allister na Jeremy Doku wa Man City.
Man City ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao kipindi cha kwanza mfungaji akiwa John Stones lakini Liverpool ilisawazisha kupitia kwa Mac Allister kwa penalti iliyotolewa baada ya kipa wa Man City kumchezea rafu Darwin Nunez.
Tukio ambalo Klopp amelilalamikia la kuinyima timu yake penalti lilipitiwa kwa kutumia VAR lakini hakuna penalti iliyotolewa kwa timu hiyo na mwamuzi wa kati hakupewa nafasi ya kulifanyia mapitio.
“Kwa nini jamaa wa chumba ch VAR anafikiri kwamba ile haikuwa penalti ya wazi na isiyo na shaka, nini hasa alichokuwa mchana,” alihoji Klopp.
“Ile ilikuwa penalti asilimia 100, wao (maofisa) watakuwa na ufafanuzi, ilikuwa faulo kwa asilimia 100 katika maeneo yote ya uwanja na pengine ingetolewa kadi ya njano, kuna mtu atalazimika kuniambia ni vipi haikuwa penalti,” alisema Klopp.
Alifafanua kuwa huenda Howard (Webb bosi wa waamuzi) atanipigia kesho na kuniambia samahani, kwa kuwa anaamini kuna mambo mawili yatakayotokea na yote hayawezi kubadili matokeo ya mchezo.
Klopp pia alisema kwamba pamoja na tukio hilo lakini jambo la kujivunia ni kwamba watu wataendelea kushuhudia soka la kuvutia ambalo tayari limeoneshwa na wachezaji wa timu yake.