Na mwandishi wetu
Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Murtaza Mangungu amesema si kweli kuwa mwekezaji wao, Mohammed Dewji ‘Mo’ aliinunua klabu hiyo miaka mitano iliyopita kama ilivyoelezwa hivi karibuni.
Mangungu alipokuwa akizungumza na kituo cha redio cha EFM Jumatano hii, alisema: “Simba SC ipo, kitu ambacho kimejitokeza ni kwamba nadhani ni uelewa wa watu wengi hata Wanasimba wenyewe kuhusu mabadiliko yaliyofanyika ndani.
“Simba SC kama ilivyo kwa timu nyingine ilikuwa inaendeshwa kwa mfumo wa ridhaa baada ya mabadiliko ya maendeleo na changamoto nyingi za kiuendeshaji, Mohammed Dewji ni mmoja wa waliojitolea sana kuisaidia klabu,” alisema Mangungu.
Alieleza kuwa Dewji kipindi ambacho hakuwa sehemu ya Simba alikuwa anatoa michango yake kama watu wengine wanaochangia lakini baadaye akatoa wazo la kutengeneza mfumo ambao watawekeza ili klabu iwe ya kiushindani zaidi
“Hivyo kwa makubaliano ya awali tuliunda chombo ambacho kiliitwa Simba SC Company Limited, ambayo ndio ambayo imegawanya muundo wa shea wa asilimia 51/49 ambapo mwanzoni ilikuwa 50/50.
“Lakini masharti yaliyowekwa na serikali yalilazimisha kuwa lazima upande wa wanachama uwe wenye hisa nyingi chombo hicho kipo na kwa uelewa wangu na ndivyo ukweli ulivyo,” alisisitiza Mangungu.
Aliongeza kuwa kuna makubaliano ya uendeshaji na Simba SC imetoa mali zake na nguvu zake kuwekeza na mwekezaji amewekeza fedha ambazo zitakuwa mtaji unaounganishwa kwa pamoja kwa ajili ya kuendesha klabu na mambo mengine.
“Mchakato huo umeanza na umefikia hatua za mwisho kwa maana kwamba kwa kuwa klabu yetu ilikuwa inaendeshwa kwa ridhaa kuna taratibu zilikuwa zinapaswa kufikiwa kwa mujibu wa taratibu za kiserikali kwa upande wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ambayo ni Wizara pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na upande wa FCC (Tume ya Ushindani).
“Maana mtaji ukizidi Shilingi bilioni tano lazima FCC wasimamie huo mchakato, hivi sasa tuko hatua ya mwisho ya kuingiza mali zetu, Simba ina bodi ya udhamini ambao ndio walioingia mkataba na mwekezaji mwenza ambaye ni Dewji,” alisema Mangungu.
Alisema baada ya kukamilisha hayo ndio wanaenda FCC kuangalia kama kila kitu ambacho kilichotakiwa kimekamilika ndipo mchakato ukamilike.
Soka Mangungu akana Mo kuinunua Simba
Mangungu akana Mo kuinunua Simba
Read also