Na mwandishi wetu
Katibu Mkuu wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), Rose Mkisi ameandika barua ya kujiuzulu nafasi yake baada ya sakata la kuishutumu serikali kwa madai ya kuupendelea zaidi mchezo wa soka.
Rose alinukuliwa na kituo kimoja cha redio hivi karibuni akisema Serikali inapendelea sana mpira wa miguu na kwamba wameisahau michezo mingine, ikiwemo netiboli (mpira wa pete).
Katibu huyo alifafanua Jumatano hii kuwa aliandika barua hiyo kwa maslahi mapana ya maendeleo ya mchezo wa netiboli na amefanya hivyo bila kushurutishwa na mtu yeyote.
“Mimi ni mtumishi wa umma, Waziri ni bosi wangu, anapotoa maagizo lazima niyafuate kwani ni bosi wangu lakini tangu alipotoa maagizo niitwe Kamati ya Nidhamu hadi leo sikupata wito.
“Nimeamua kukaa pembeni ili kutotia doa kwani nimefanya kila kitu kwa ajili ya kuupeleka mbali mchezo wa netiboli lakini naamini muda umefika wa kukaa pembeni wengine waendelee nilipoishia,” alisema Rose na kuongeza:
“Nimeamua kujiuzulu nafasi ya katibu mkuu kutokana na sintofahamu kuhusu maandalizi ya timu ya mpira wa pete inayojiandaa kushiriki mashindano ya wanawake chini ya miaka 21 yanayotarajia kufanyika nchini Afrika Kusini. Nimefikia maamuzi haya kwa masalahi mapana ya taifa na maendeleo ya mpira wa pete nchini.” alisema Mkisi.
Wakati huohuo, Chaneta imeomba radhi na kuiomba serikali kuwarejeshea huduma zote ilizokata baada ya kauli ya Rose ya kudai kuwa serikali imekuwa ikiupendelea zaidi mchezo wa soka kuliko mingine.
Mwenyekiti wa Chaneta, Dk Devota Marwa alisema kuwa wanakiri kwamba kauli iliyotolewa na katibu wao haikuwa ya chama.
Alifafanua kuwa hadi kauli hiyo inatolewa serikali ilikuwa imekubali ombi la kusaidia gharama zote za safari ya timu ya taifa chini ya miaka 21 itakayoenda Afrika Kusini kwa mechi ya kufuzu Kombe la Dunia.