Na mwandishi wetu
Baada ya kuongoza kwenye mbio za ufungaji bora Ligi Kuu NBC, kiungo wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amesema hatolei macho tuzo ya ufungaji bora badala yake lengo lake namba moja ni kuisaidia timu yake kubeba taji la ligi kuu.
Mabao mawili aliyoyafunga Jumapili katika mechi dhidi ya Dodoma Jiji FC, yamemfanya kiungo huyo kufikisha mabao 11 na kumpita kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki mwenye mabao 10.
Akizungumza baada ya mchezo huo kiungo huyo alisema siri ya kiwango chake kupanda ni kujituma na kufuata maelekezo ya kocha wake na lengo kubwa ni kuona Azam inabeba ubingwa wa ligi msimu huu.
“Mabao ninayofunga ni kwa ajili ya kuisaidia timu yangu na si kwamba nataka kushindana na mtu hapa, namheshimu Aziz Ki ni mchezaji mkubwa lakini watu wajue kila zuri ninalofanya lengo ni kuipigania timu yangu,” alisema Fei Toto.
Kiungo huyo wa zamani wa Yanga, alisema anajua ligi imekuwa na ushindani mkubwa lakini wataendelea kupambana ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri na kutimiza lengo hilo ambalo wamekusudia kulifikia msimu huu.
Azam ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikikusanya pointi 43 sawa na vinara Yanga, lakini Azam ipo mbele kwa michezo mitatu dhidi ya Yanga na michezo minne dhidi ya wanaoshika nafasi ya tatu Simba SC.