Na mwandishi wetu
Uongozi wa timu ya Singida Fountain Gate umebariki kuondoka kwa aliyekuwa kiungo wao, Bruno Gomes (pichani) lakini umeahidi kuisuka upya timu hiyo ili msimu ujao irudi kwenye ushindani.
Gomes alieleza jana Jumatatu kumalizana na klabu hiyo kwa madai ya kukiukwa kwa baadhi ya vitu kwenye mkataba wake jambo ambalo hajapendezwa nalo.
Makamu Mwenyekiti wa Singida, John Kadutu alisema kuna mambo mengi wamekusudia kuyafanya kwenye kikosi chao ikiwemo usajili wa nguvu ili kuiimarisha timu hiyo ili irudi katika ushindani iliyokuwa nao hapo awali.
“Unajua tangu kuanza mzunguko wa pili tumekuwa na mwenendo mbaya na hiyo imetokana na mambo mengi kutokuwa sawa ikiwemo baadhi ya wachezaji muhimu kuondoka na jana (leo) Bruno ameomba kuondoka, tumeridhia,” alisema Kadutu.
Kiongozi huyo alisema mikakati yao ni kukisuka upya kikosi chao ili msimu ujao warudi kiushindani zaidi kama ilivyokuwa mwanzoni mwa msimu huu.
Singida imeendelea kuporomoka kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC kwa sasa inashika nafasi ya nane ikiwa na pointi 21 katika michezo 19 iliyocheza hadi sasa.
Pia haijafahamika kiungo huyo Mbrazili aliyejiunga na Singida misimu miwili iliyopita anakwenda wapi ambapo licha ya msimu uliopita kufanya vizuri kwa kufunga mabao 10 na kuzivutia Simba na Yanga lakini msimu huu ameshindwa kuwika kutokana na majeraha ya mara kwa mara, akifunga bao moja pekee mpaka sasa.