Madrid, Hispania
Klabu ya Real Madrid ya Hispania inajipanga kukata rufaa dhidi ya kadi nyekundu aliyopewa kiungo wake Jude Bellingham katika mechi dhidi ya Valencia iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Jumamosi iliyopita, Bellingham alipewa kadi hiyo baada ya kuibuka mzozo baina ya wachezaji na maofisa wa Real Madrid dhidi ya mwamuzi wa mechi hiyo, Gil Minzano.
Habari zaidi zinadai kwamba ripoti ya Ginzano ilieleza kuwa Bellingham alitoa lugha kali dhidi ya mwamuzi zaidi ya mara moja kwa kile alichoamini kuwa mwamuzi huyo aliinyima timu yake bao ambalo lingewawezesha kutoka na ushindi wa 3-2.
Alichokuwa akikipinga Bellingham ni hatua ya mwamuzi huyo, Gil Minzano kupuliza filimbi ya kumaliza mchezo wakati alipopiga mpira wa kichwa uliotokana na krosi ya Brahim Diaz na kujaa wavuni katika dakika ya tisa ya dakika za nyongeza.
Baada ya mechi hiyo, kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti alimtetea Bellingham akisema kwamba mchezaji huyo hakutamka neno lolote la kumtusi mwamuzi wa mchezo huo.
“Tumeumizwa na kadi nyekundu aliyopewa Bellingham, hakutoa kauli yoyote ya kumtukana mwamuzi, alitoa kauli ya kulalamika kunyimwa goli kama ambavyo sisi sote tulikuwa katika fikra za aina hiyo,” alisema Ancelotti.
Bellingham alipewa kadi hiyo wakati mpira ukiwa umekwisha na kwa mujibu wa Ancelotti, mwamuzi alikosea na kusisitiza kwamba mchezaji wake alikuwa sahihi kwa kile alichokuwa akikilalamikia.