Manchester, England
Mshambuliaji wa Man United, Marcus Rashford amewataka watu wanaotilia shaka uwajibikaji wake katika klabu hiyo wawe na ubinadamu.
Rashford, 26, hadi sasa ameifungia Man United mabao matano msimu huu hali ambayo inadaiwa kusababisha ajikute akishutumiwa hasa kutokana na tabia zake.
Mshambuliaji huyo alikosekana kwenye mechi ya Kombe la FA dhidi ya Newport ikiwa ni siku chache baada ya kuonekana akiwa katika klabu moja ya usiku Ireland ya Kaskazini.
“Kama mtakuwa mnahoji uwajibikaji wangu kwa United hapo ndipo mtakaponilazimisha nizungumze, ni sawa na mtu kuhoji utambulisho wangu na kila kitu ninachokisimamia kama mwanaume” alisema Rashford.
“Nimekulia hapa, nimecheza katika klabu hii tangu nikiwa kijana mdogo, familia yangu ilikataa pesa ambazo zingeweza kubadili maisha ili tu nivae nembo ya klabu hii,” alisema Rashford.
Rashford ambaye ni mzaliwa wa jiji la Manchester, ameanzia kucheza soka katika timu ya vijana ya Man United kabla ya kucheza katika kikosi cha kwanza mwaka 2016 akiwa na miaka 18 na hadi sasa ameichezea timu hiyo mechi 391 na kuifungia mabao 128.
Msimu uliopita ulikuwa mzuri kwa Rashford ambaye aliifungia Man United mabao 30 na ilitarajiwa msimu huu ungekuwa mzuri zaidi kwake lakini hali imekuwa tofauti hadi sasa na kujikuta akisakamwa mara kwa mara.
“Naweza kupokea shutuma zozote, popote ikiwamo vichwa vya habari vya mitandaoni na magazetini, naweza kuyapokea yote, lakini unapohoji uwajibikaji wangu katika klabu hii na mapenzi yangu katika soka na kuiingiza familia yangu, hapo nitalazimika kukutaka kidogo uwe na ubinadamu,” alisema Rashford.