Madrid, Hispania
Rais wa Ligi Kuu Hispania au La Liga, Javier Tebas amesema anatumaini mshambuliaji wa Man United, Mason Greenwood anayecheza kwa mkopo katika klabu ya Getafe atabaki Hispania hata baada ya muda wake wa mkopo kufikia mwisho.
Greenwood alijiunga na Getafe, Septemba mwaka jana baada ya Man United kubadili uamuzi wa awali wa kumtaka abaki katika klabu hiyo licha ya kuandamwa na kashfa ya kumdhalilisha mwanamke.
Man United walitangaza kufanya uchunguzi wa ndani baada ya Greenwood kufutiwa kesi ya udhalilishaji na kukawa na dalili za mchezaji huyo kubaki katika klabu hiyo lakini jambo hilo lilikumbana na vikwazo kadhaa na hivyo ikaonekana bora kumuuza kwa mkopo.
Akizungumzia suala la Greenwood, Tebas alisema yeye kama mwanasheria hana sababu ya kuhoji mambo yaliyopita ya mchezaji huyo kuhusu mashtaka yaliyokuwa yakimkabili kufutwa badala yake anachofahamu ni kwamba amekutwa hana hatia
“Mimi ni mwanasheria, kama mtu anapitia mahakamani kisheria na kukutwa hana hatia, hapo hakuna zaidi la kuzungumza,” alisema Tebas.
Tebas alimsifia Greenwood akisema kwamba anafanya vizuri na anaamini ataendelea kucheza soka la Hispania kwani jambo hilo pia ni zuri kwao La Liga.
Alipobanwa zaidi kuhusu sakata la udhalilishaji linalomkabili mchezaji huyo, Tebas alisema kwamba kama mchezaji huyo hakuadhibiwa huko, si jukumu la La Liga kumchukulia hatua za kisheria.
“Ni lazima mheshimu mifumo ya kisheria, watu wanaweza kumshutumu kwenye vyombo vya habari lakini mna ulazima wa kuheshimu maamuzi wa kimahakama, hakuna la kuzungumza zaidi ya hilo,” alisema Tebas.