Na mwandishi wetu
Mwili wa daktari wa zamani wa klabu ya Azam, Mwanandi Mwankemwa unatarajiwa kuzikwa leo Alhamisi kwenye makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam baada ya sala ya alasiri.
Mwankemwa ambaye pia aliwahi kuwa daktari wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, timu za Olimpiki, michezo ya Afrika, Jumuiya ya Madola za Tanzania na JKT Ruvu alifariki kwa tatizo la moyo Jumatatu iliyopita katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, Dar es Salaam.
Akizungumza na GreenSports Jumatano hii, meneja habari na mawasiliano wa Azam FC, Zakaria Thabiti ‘Zaka Zakazi’, alisema msiba upo Mwanagati nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam na taratibu zote zinakwenda vizuri.
“Msiba upo nyumbani kwake Mwanagati na tunatarajia atazikwa katika makaburi ya Kinondoni, na maiti itaswaliwa Msikiti Mkuu wa Bakwata, Kinondoni, Dar es Salaam,” alisema.
Mwankemwa ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha Madaktari wa Michezo (Tasma), amehudumu Azam FC kwa miaka 16 tangu timu hiyo ilipopanda daraja mwaka 2008 na aliingia katika udaktari michezoni mwaka 1982 na wakati huo akiwa na timu ya JKT Ruvu.