Na mwandishi wetu
Simba inachofikiria ni mechi yao na Jwaneng Galaxy, baada ya kurejea kutoka Ivory Coast, kikosi cha timu hiyo kimepitiliza kambini moja kwa moja kuanza maandalizi ya mchezo huo wa mwisho wa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza Jumatatu hii kocha msaidizi Smba, Selemani Matola alisema mchezo huo utakaopigwa Mechi 2 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, ni muhimu kwani ndio umebeba hatima yao ya kuingia robo fainali kwa mara nyingine.
“Kesho tunaanza maandalizi ya mchezo wetu wa mwisho ambao ni kama fainali, kuna mambo mawili katika mechi dhidi ya Jwaneng Galaxy kutafuta ushindi utakaotupeleka hatua ya robo fainali na kulipa kisasi.
“Hii haitakuwa mechi ya kawaida bali ni kama fainali kwetu kuhakikisha tunafikia malengo yetu ya kwenda robo fainali kwa kumfunga mpinzani wetu,” alisema Matola.
Wakati huohuo, ofisa habari wa Simba, Ahmed Ally ametangaza kuwa kauli mbiu ya mchezo wao wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ni Vita ya Kisasi.
Alisema lengo la kauli mbiu hiyo ni kutaka kulipa kisasi kwa Jwaneng kwani waliwahi kuwatoa katika raundi ya kwanza ya michuano hiyo misimu miwili iliyopita.
“Tunakumbuka mwaka 2021 Jwaneng walitutoa kwenye michuano hii, ndio maana tunasema ni Vita ya Kisasi kwa kuwa tunataka kuwapa huzuni kama walivyofanya kwetu.
“Faida za kushinda katika mchezo huu ni tatu ambazo ni kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kulipa kisasi na kuwa timu ya tano kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya nne mfululizo,” alisema Ahmed.