Na mwandishi wetu
Yanga leo Jumamosi imefurahia Pacome Day kwa kufuzu kwa kishindo hatua ya robo fanali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiichapa CR Belouizdad ya Algeria mabao 4-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Baada ya mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa Belouizdad, Yanga ilifungua ukurasa wa mabao dakika ya 44 kwa bao lililofungwa na Mudathir Yahya aliyeunganisha pasi ya chinichini ya Pacome Zouazoua.
Kama kawaida yake Mudathir aliendelea kulifurahia bao hilo kwa staili ya kuongea na simu akitumia kilinda ugoko kujifanya kama mtu anayewasiliana na simu.
Dakika moja baada ya kuanza kipindi cha pili Yanga iliandika bao la pili lililofungwa na Aziz Ki aliyeitumia pasi ya Pacome na kabla Belouizdad hawajatulia walichapwa bao la tatu lililofungwa na Kennedy Musonda.
Musonda alifunga bao hilo kutokana na juhudi binafsi za Pacome ambaye aliambaa na mpira kabla ya kumchambua beki na kipa wa Belouizdad, Alex Gunduz mara mbili na kumuunganishia pasi mfungaji.
Kuingia kwa bao hilo kuliwaamsha Belouizdad ambao walianza kulisakama lango la Yanga lakini uimara wa safu ya ulinzi ya Yanga ukiongozwa na kipa Djigui Diarra aliyekuwa mkali kwa kuipanga safu hiyo ulikuwa kikwazo kwa Belouizdad kupata bao.
Belouizdad wakati wakiendelea kulisakama lango la Yanga walijisahau na kujikuta wakipachikwa bao la nne lililofungwa na mshambuliaji mpya wa Yanga, Joseph Guede aliyeitumia pasi ya Aziz Ki.
Katika tukio la kushangaza mmoja wa wachezaji wa Belouizdad aliingia kwenye mzozo na kocha wake japo wachezaji na viongozi waliokuwa karibu walifanikiwa kuwatuliza na tukio hilo kudumu muda mfupi.
Katika mechi ya leo baadhi ya wachezaji nyota wa Yanga wakiongozwa na Pacome waliingia uwanjani nywele zao zikiwa zimepakwa rangi ya njano staili maarufu ambayo zimezoeleka kutumiwa zaidi na Pacome.
Kimataifa Yanga yaibugiza Belouizdad 4-0
Yanga yaibugiza Belouizdad 4-0
Read also