Na mwandishi wetu
Timu ya soka ya taifa ya wanawake, Twiga Stars itashuka kwenye dimba la Azam Complex Ijumaa hii kuikabili Afrika Kusini, ‘Banyana Banyana’ katika mchezo wa kuwania kufuzu Michezo ya Olimpiki.
Mchezo huo ni muhimu kwa Twiga kushinda nyumbani ili kujiweka kwenye mazingira mazuri pindi timu hizo zitakaporudiana Februari 27, mwaka huu nchini Afrika Kusini.
Twiga imefuzu kushiriki michuano ya mataifa ya Afrika kwa Wanawake, Wafcon 2024 itakayofanyika Morocco baada ya kushindwa kushiriki kwa zaidi ya miaka 10, hivyo kufuzu huko kunatoa matumaini ya kuendeleza ushindi kwa Banyana na kuendeleza ari waliyonayo kuelekea Wafcon.
Wachezaji wa Twiga Stars; Fatma Issa na Stumai Abdallah wakiuzungumzia mchezo huo dhidi ya mabingwa watetezi hao wa Wafcon walisema wamejiandaa vizuri na wako tayari kupambana kumaliza mechi nyumbani.
“Kitu ambacho tulikuwa tukizungumza na wenzangu ni kupambana kwa sababu tunajua ni mchezo mgumu sana na kila mchezaji ana morali ya kutosha, wajitokeze kwa wingi mashabiki na sisi tutawafurahisha,” alisema Fatma.
“Nina imani kocha wetu anajua cha kufanya, tukimaliza mechi nyumbani ugenini hatutapata shida, Mungu atatusaidia na kwa juhudi zetu wenyewe pia tutashinda,” alisema Stumai.