Barcelona, Hispania
Mahakama nchini Hispania imemkuta na hatia ya kosa la kubaka beki wa zamani wa Barcelona na timu ya taifa ya Brazil, Dani Alves na kumhukumu kifungo cha miaka minne na nusu jela.
Alves, 40, anadaiwa kufanya kosa hilo Desemba 31, 2022 katika klabu moja ya usiku ingawa mchezaji huyo amekana kumfanyia udhalilishaji msichana aliyemshitaki.
Mwanasheria wa Alves hata hivyo ameahidi kuikatia rufaa hukumu hiyo wakati mwanasheria wa msichana anayedaiwa kubakwa alisema walikuwa wakiujua ukweli wa alichofanyiwa mshitaki na adha aliyokumbana nayo.
Mahakama hiyo mbali na kumhukumu beki huyo ambaye pia amejipatia mafanikio na klabu mbalimbali za soka barani Ulaya, pia imeahidi kumpa adhabu nyingine ya kuwa chini ya uangalizi kwa miaka mitano.
Waendesha mashitaka katika kesi hiyo walitaka Alves afungwe jela miaka tisa kwa kuwa makosa ya aina hiyo kwa sheria za Hispania adhabu yake inaanzia kifungo cha miaka minne hadi 15 jela.
Mahakama hiyo pia ilikataa hoja ya mwanasheria wa Alves aliyedai kwamba mteja wake alitakiwa kupewa adhabu ndogo kwa sababu siku anayodaiwa kufanya kitendo cha ubakaji alikuwa amelewa.
Mke wa Alves, Joana Sanz naye alijenga hoja hiyo akidai kwamba mumewe alionekana kuwa katika hali ya ulevi aliporudi katika makazi yao mjini Barcelona usiku wa siku anayodaiwa kubaka, alipofika alivunja baadhi ya samani za kwenye nyumba kabla ya kuangukia kitandani.
Katika kupingana na hoja hiyo, mahakama ilidai kwamba kiwango cha pombe alichokunywa mchezaji huyo hakikuathiri tabia zake.
Awali waendesha mashitaka waliieleza mahakama kuwa, Alves na rafiki yake wakiwa katika klabu ya usiku waliwanunulia pombe kali wasichana watatu lakini baadaye, Alves alimrubuni mmoja wao na kwenda naye eneo la VIP ambalo lina choo jambo ambalo msichana huyo hakufahamu.
Kwa mujibu wa wasichana hao, wakiwa katika eneo hilo Alves alianza kuonesha ukatili na kumbaka mwenzao licha ya msichana huyo kumsihi asifanye hivyo lakini Alves hakumsikiliza.
Kimataifa Dani Alves jela miaka minne kwa kubaka
Dani Alves jela miaka minne kwa kubaka
Read also