Rio de Janeiro, Brazil
Kocha wa timu ya taifa ya Brazil, Dorival ambaye aliwahi kusema kwamba Brazil ianze kufikiria maisha bila ya Neymar, amebadili kauli hiyo na sasa anasema Neymar ataendelea kuwa mchezaji muhimu kwenye timu ya taifa.
Neymar, 32 anayekipiga Al Hilal ya Saudi Arabia, aliumia goti la mguu wa kushoto wakati akiiwakilisha timu ya taifa ya Brazil Oktoba mwaka jana na hadi sasa anaendelea na matibabu na ameonesha dalili za kupona na kurudi uwanjani.
Akimzungumzia mchezaji huyo, Dorival alinukuliwa mwezi uliopita akisema ingawa Neymar ni kati ya wachezaji bora watatu duniani lakini Brazil inalazimika kujifunza kucheza bila ya mchezaji huyo.
Kwa sasa Dorival si tena mwenye imani hiyo baada ya kunukuliwa hivi karibuni akisema kwamba Neymar ana nafasi katika mipango yake kwenye kikosi cha Brazil.
Dorival aliulizwa kuhusu kupona kwa Neymar naye akasema,”Ni kati ya mambo muhimu, Neymar ni mchezaji muhimu sana, hilo hata yeye analifahamu, ni kati ya wachezaji bora duniani.”
“Matumaini yetu ni kwamba atapona, atakuwa vizuri, bado ana nafasi (kwenye kikosi) kwa kila ambacho amekifanikisha katika timu ya taifa lakini anahitaji kujiamini, kutulia na kuwa vizuri na zaidi ya yote kuwa makini, atakuwa sehemu ya mpango wetu kama atakuwa fiti,” alisema Dorival.
Tangu aanze kuichezea timu ya taifa ya Brazil, Agosti 2010, Neymar hadi sasa ndiye kinara wa mabao wa timu akiwa na rekodi ya kuifungia jumla ya mabao 79 katika mechi 128