Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amefurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake na kupata ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Ushindi huo umeifanya Yanga kutinga 16 bora ya michuano ya Kombe la FA (ASFC) na kuungana na Kagera Sugar, Rhino Rangers, Mashujaa na KMC ambazo pia zimetinga hatua hiyo.
“Tulikuwa na muunganiko mzuri hiyo ndio tofauti ya Yanga na timu nyingine, nimefurahishwa na kiwango kilichooneshwa na wachezaji Augustine Okrah na Joseph Guede, wako kwenye mchakato wameingia kikosini kwenye dirisha dogo.
“Wanahitaji muda mfano Guede ni mshambuliaji lakini anapokuwa hafungi anavunjika moyo lakini amefunga mabao mawili mazuri kitu ambacho naamini kinampa hali ya kujiamini zaidi,” alisema Gamondi.
Kocha huyo pia alizungumzia mchezo wao ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya timu ya CR Belouizdad.
“Mchezo wetu dhidi ya Belouizdad ni mechi kubwa ambayo ni lazima tushinde ili kujiweka kwenye nafasi nzuri na tumeanza maandalizi ya mchezo huu kwani Belouizdad ni miongoni mwa timu kubwa yenye historia nzuri kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa.”
Aliongeza kuwa mwanzo malengo yao yalikuwa kufuzu hatua ya makundi na wamepambana vizuri na kwamba kwa sasa hawezi kuwapa presha wachezaji wake zaidi ya kupambana ili kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo wa marudiano wa hatua ya makundi.
Soka Kiwango Yanga chamfurahisha Gamondi
Kiwango Yanga chamfurahisha Gamondi
Read also