Na mwandishi wetu
Kipa namba moja wa KMC, Wilbol Maseke amewaomba radhi mashabiki kwa kitendo cha kumrushia ngumi mchezaji mwenzake, Ibrahim Mao kwenye mchezo wa Ligi Kuu NBC dhidi ya Yanga uliochezwa hivi karibuni kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.
Tukio hilo lilitokea baada ya KMC kufungwa bao la kwanza dakika za mapema kutokana na makosa ya Maseke na kumfanya aendelee kufanya makosa mengi ndipo Ibrahim Mao akaenda kumshauri atulie na kusababisha ugomvi huo.
Dakika ya 46, KMC ilifanya mabadiliko ya kipa kwa kumtoa Maseke na nafasi yake ikachukuliwa na Denis Richard katika mchezo huo ulioisha kwa Yanga kutoka uwanjani na ushindi wa mabao 3-0.
Maseke ametumia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram kuomba radhi kwa kilichotokea kuwa si cha kimichezo baada ya mchezo huo.
“Poleni mashabiki zangu na wanaopenda kazi ninayofanya nikiwa uwanjani, niombe radhi kwa kitendo kilichojitokeza mimi kugombana na mwenzangu.
“Haikuwa kusudio langu, pia baada ya hapo ukweli ni kwamba sikuendelea na ugomvi kwenye vyumba vya kubadilishia nguo bali yale ni maamuzi ya mwalimu kunitoa na nimeheshimu hilo,” alisema Maseke.
Maseke aliongeza kuwa ana mengi ya kusema ambayo huwa yanaendelea nje ya uwanja ambayo yalisababisha kuharibu saikolojia yake lakini akaomba wamsamehe kwa kilichotokea.