London, England
Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp amempongeza kocha wa Bayer Leverkusen ya Ujerumani, Xabi Alonso (pichani) akidai kuwa ni kocha wa kizazi kipya.
Mwezi uliopita, Klopp alitangaza atang’atuka kuinoa Liverpool mwishoni mwa msimu huu na Alonso, kiungo wa zamani wa Liverpool aliyeichezea timu hiyo kati ya mwaka 2004 na 2009, jina lake linatajwa kuwa ni kocha anayefaa kumrithi Klopp.
Alonso, 42 ambaye pia ni kiungo wa zamani wa timu ya taifa ya Hispania kwa sasa anainoa Leverkusen ambayo inashika usukani katika Ligi Kuu Ujerumani au Bundesliga ikiwa mbele ya vigogo Bayern Munich inayoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi tano.
Zaidi ya mafanikio hayo yanayoonekana kwenye Bundesliga, Alonso pia ameweka rekodi ya kucheza mechi 31 za mashindano yote bila kupoteza hata moja na hivyo amebakisha mechi moja kuweka rekodi iliyowahi kuwekwa na Bayern ya mechi 32 bila kupoteza.
“Xabi anafanya kazi nzuri, hili ni langu binafsi (halimhusishi na Liverpool) ni mchezaji wa zamani wa hadhi ya juu duniani na anayetokea katika familia ya ukocha jambo ambalo pia linasaidia, ni kama vile tayari alishakuwa kocha wakati akicheza soka,” alisema Klopp.
Alonso hata hivyo alipoulizwa juu ya uwezekano wa kumrithi Klopp katika klabu ya Liverpool, aliamua kujiweka kando na hoja hiyo akisema kwamba kwa sasa anaifikiria Leverkusen tu.
Akiwa mchezaji wa Liverpool, Alonso alibeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na FA na kazi ya ukocha katika kiwango cha juu aliianza Oktoba, 2022 katika klabu ya Leverkusen ambayo ameendelea kuwa nayo hadi sasa.