Seoul, Korea Kusini
Kocha Jurgen Klinsmann aliyekuwa akiinoa timu ya taifa ya Korea Kusini, ametimuliwa katika nafasi hiyo ikiwa imepita miezi 12 tangu akabidhiwe jukumu hilo.
Uamuzi wa Korea Kusini kumtimua Klinsmann unahusishwa moja kwa moja na hatua ya timu hiyo kuishia nusu fainali ya Kombe la Asia baada ya kushindwa kutamba mbele ya Jordan.
Klinsmann, 59, alikabidhiwa majukumu ya kuinoa timu hiyo Februari mwaka jana kwa mkataba ambao ulitarajiwa kufikia mwisho mwaka 2026 baada ya fainali za Kombe la Dunia.
Korea Kusini ambayo inahaha kwa zaidi ya miaka 60 ikiwania kubeba Kombe la Asia ilichukua uamuzi huo na chama cha soka cha nchi hiyo kiliweka wazi kutoridhishwa na aina ya uongozi wa Klinsmann na kwamba mabadiliko lilikuwa jambo muhimu.
Mashabiki na baadhi ya wanasiasa wa Korea Kusini mara baada ya timu hiyo kutolewa kwenye Kombe la Asia wamekuwa wakitaka kocha huyo atimuliwe huku kukiwa na madai ya ugomvi baina ya wachezaji wa timu hiyo.
Habari za ndani zinadai kuwa nahodha wa timu ya Korea Kusini, Son Heung-min aliumia kidole baada ya kutokea ugomvi na mchezaji mwenzake wakati wa chakula cha jioni kabla ya timu hiyo kupoteza mechi yake na Jordan.
Inaaminika kuwa malalamiko hayo ndiyo yaliyokishawishi Chama cha Soka Korea Kusini (KFA) kutangaza kuachana na kocha huyo kutoka Ujerumani, kocha ambaye iliaminika angekwenda na timu hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026.
Klinsmann pia alikuwa akilalamikiwa kwa kitendo chake cha kutopenda kuishi Korea Kusini badala yake alikuwa akitumia muda mwingi katika makazi yake California nchini Marekani wakati makocha wengine wa kigeni waliishi mjini Seoul.
Kimataifa Klinsmann atimuliwa Korea Kusini
Klinsmann atimuliwa Korea Kusini
Related posts
Read also