Na mwandishi wetu
Licha ya Simba kuachwa kwa tofauti ya pointi nne na mahasimu wao Yanga wanaoongoza Ligi Kuu NBC, kiungo wa timu hiyo, Clatous Chama amesema bado wako kwenye mbio za kuwania ubingwa msimu huu wa 2023-24.
Chama alisema hayo baada ya kufunga bao muhimu lililoisaidia timu yake kupata ushindi wa bao 1-0 jana ugenini dhidi ya JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam.
Kiungo huyo ambaye amefunga mabao mawili na kutoa ‘asisti’ mbili katika mechi nne za Simba tangu arejee baada ya kuitumikia Zambia kwenye Afcon, alisema mzunguko wa kwanza haukuwa mbaya.
Alifafanua kwamba walianza kwa kuchechemea na kufanya makosa madogo lakini bado wanaendelea kujitafuta na kurekebisha makosa ili waimarike na kutimiza malengo yao.
“Nafasi ya pili siyo mbaya, wanaoongoza wametuzidi pointi nne, tutapambana tuendelee kuona tutafika wapi lakini malengo yetu ni kushinda ubingwa wa ligi kuu.
“Hivi sasa siangalii sana ufungaji bora wa ligi kuu, muhimu ni timu kwanza ifanye vizuri halafu mimi. Kutakuwa hakuna umuhimu wa kuwa mfungaji bora halafu timu haijabeba ubingwa,” alisema Chama.
Simba iko nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 36 baada ya kushuka uwanjani mara 15 ikiwa imeshinda michezo 11, sare tatu na kufungwa mechi moja.