Na mwandishi wetu
Simba leo imeendelea kuifukuzia Yanga kwenye Ligi Kuu NBC baada ya kutoka na ushindi wa bao 1-0 mbele ya JKT Tanzania katika mechi ya ligi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.
Kwa ushindi huo, Simba sasa inakuwa imefikisha pointi 36 katika mechi 15 ikiwa nafasi ya pili na hivyo inakuwa imezidiwa na mahasimu wake Yanga wanaoongoza ligi hiyo kwa tofauti ya pointi nne tu na timu zote hizo zimecheza idadi sawa ya mechi hadi sasa.
Kwa mara nyingine alikuwa ni Clatous Chota Chama aliyewainua vitini mashabiki wa Simba kwa bao hilo pekee katika dakika ya 33 akiitumia vizuri pasi ya Saido Ntibazonkiza.
Hii ni mara ya pili kwa Chama kuifungia Simba bao muhimu katika mechi za hivi karibuni za Ligi Kuu NBC, mara ya mwisho alifanya hivyo katika mechi dhidi ya Azam FC na kuiwezesha Simba kutoka sare ya bao 1-1.
Simba na JKT kwa kipindi kirefu cha mchezo zote zilionesha uhai na uchu wa kusaka bao na JKT wangeweza kupata bao la kusawazisha katika dakika ya 68 lakini Ismail Aziz alishindwa kuitumia nafasi ambayo timu hiyo iliitengeneza kwa kupiga shuti ambalo kipa wa Simba, Ayoub Lakred alilidaka.
Ligi hiyo itaendelea kesho Ijumaa ambapo Azam watakuwa nyumbani Azam Complex kuumana na Geita Gold wakati Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa Mashujaa FC kwenye Uwanja wa Kaitaba.
Soka Simba yaipiga JKT, yaisogelea Yanga
Simba yaipiga JKT, yaisogelea Yanga
Read also