Na mwandishi wetu
Simba imeipiku Azam FC katika Ligi Kuu NBC kwa kuchupa hadi nafasi ya pili baada ya ushindi wa bao 1-0 ilioupata katika mechi yake na Geita Gold iliyopigwa Jumatatu hii kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha pointi 33 katika mechi 14 ikiwa imeizidi Azam inayoshika nafasi ya tatu kwa tofauti ya pointi moja wakati Yanga inashika usukani ikiwa na pointi 40 katika mechi 15.
Msimamo wa ligi hiyo pia unaonesha kuwa KMC inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 21 wakati Singida Fountain Gate (Singida FG) inakamilisha top five ikiwa na pointi 20.
Bao pekee lililoibeba Simba katika mechi hiyo lilipatikana dakika ya 81 mfungaji akiwa ni mchezaji mpya wa timu hiyo Babacar Sarr ambaye aliitumia pasi ya Kibu Dennis Prosper.
Geita ambao walipambana vizuri na kuzuia mashambulizi ya Simba kwa kipindi kirefu lakini walipoteza umakini na kujikuta wakipachikwa bao ambalo lilisakwa kwa udi na uvumba na wachezaji wa Simba.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo zilizochezwa Jumatatu hii, Mtibwa Sugar ililala kwa mabao 3-2 mbele ya Ihefu FC wakati Kagera Sugar iliilaza Singida FG bao 1-0 na KMC na Coastal Union zilitoka sare ya bila kufungana.
Soka Simba yailaza Geita, yaipiku Azam
Simba yailaza Geita, yaipiku Azam
Read also