Abidjan, Ivory Coast
Ivory Coast hatimaye imefanikiwa kulibakisha nyumbani taji la Afcon 2023 baada ya kuichapa Nigeria mabao 2-1 katika mechi ya fainali iliyopigwa Jumapili hii usiku mjini Abidjan.
Nigeria ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 38 lililofungwa na William Ekong na kuibua dalili zote za timu hiyo kubeba taji la nne la Afcon dhidi ya Ivory Coast waliokuwa wakisaka taji la tatu.
Hata hivyo walikuwa ni Franck Kessie aliyeisawazishia Ivory Coast bao dakika ya 62 na Sebastian Haller aliyefunga bao la ushindi dakika ya 81 na kuwafanya wenjeji kutoka katika dimba la Alassane Ouattara kwa shangwe na vigelegele.
Kwa Haller ambaye pia ni mchezaji wa Borussia Dortmund ya Ujerumani, bao hilo ni ushindi mwingine mkubwa wa pili kwake ikiwa ni takriban miezi sita imepita tangu atangaze kupona maradhi ya saratani (kansa).
Haller kwa mara ya kwanza alitangazwa kuugua kansa Julai 2022 ikiwa ni siku chache tangu aanze kufurahia maisha katika klabu ya Dortmund lakini alipata tiba sahihi na kupona na hatimaye kuendelea na soka kama kawaida.
“Tulikuwa tukiota jambo hili kwa miaka mingi, tulikuwa na matumaini ya kufikia hatua hii, na kwa mara nyingine mechi haikuwa rahisi, furaha unayoiona hapa ni kwa kile kilichotokea katika nchi hii, wana kila sababu ya kufurahi, naamini imewafanya watu wengi kuwa na furaha,” alisema Haller.
Ni Haller ambaye pia aliiwezesha Ivory Coast kufuzu hatua ya fainali baada ya kufunga bao pekee na la ushindi wakati timu hiyo ikiichapa DR Congo bao 1-0 katika mechi ya nusu fainali.
Haller ambaye ni mzaliwa wa jiji la Paris, Ufaransa lakini alichagua kuichezea nchi yake ya asili, hakutarajiwa kama angeweza kuifikisha timu hiyo hatua ya fainali hadi kubeba kombe kwa namna mwanzo ulivyokuwa mgumu.
Ivory Coast ilizianza fainali hizo vibaya ikiwamo kipigo cha mabao 4-0 mbele ya Equatorial Guinea hadi kulazimika kuchukua uamuzi mgumu wa kuachana na aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Jean-Louis Gasset.
Nafasi ya Gasset alikabidhiwa kocha wa muda, Emerse Fae ambaye hatimaye alifanikiwa kubadili upepo na kulibakisha taji la Afcon Ivory Coast.