Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamodi amesema amefurahia kuona timu yake ikipata ushindi dhidi ya Mashujaa FC, lakini hajafurahishwa na safu yake ya ushambuliaji.
Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam Alhamisi iliyopita, Yanga ilishinda mabao 2-1 na kuzidi kujichimbia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu NBC wakifikisha pointi 37 katika michezo 14.
Kocha huyo raia wa Argentina alisema washambuliaji wake ni kama wamepoteza umakini na kukosa ukatili kutokana na kushindwa kuzitumia ipasavyo nafasi nyingi wanazotengeneza katika michezo mitatu waliyocheza siku za karibuni.
“Nafurahi kuona tumekuwa bora kumiliki mchezo na kufanya mambo mengi kwa usahihi isipokuwa safu yangu ya ushambuliaji bado haijafanya kile ambacho nataka ifanye, tunapoteza nafasi nyingi kitu ambacho si kizuri hasa unapokutana na timu ambayo haikupi nafasi nyingi,”.
“Lakini pia sijafuraishwa na nama wapinzani wetu Mashujaa walivyocheza, muda wote walikuwa wapo nyuma kitu ambacho kiliwapa ugumu washambuliaji wetu kuzitumia hizo nafasi walizotengeneza na hiyo inapoteza ladha ya mchezo wa soka,” alisema Gamondi.
Naye kocha mkuu wa Mashujaa, Mohamed Abdallah ‘Baresi’ alisema: “Hongera kwa Yanga kwa ushindi walioupata lakini niseme tulikuwa kwenye kiwango bora pengine kuliko mechi zote tulizocheza msimu huu, kupoteza umakini dakika za mwisho ndio kumewapa bao wapinzani, tumekubali tunarudi nymbani kujipanga kwa mechi nyingine,” alisema Beresi.