Na mwandishi wetu
Kiungo mshambuliaji mpya wa Yanga, Augustine Okrah ameushukuru uongozi na jopo la madaktari wa Yanga kwa kumpatia huduma bora iliyomuwezesha kurudi uwanjani haraka.
Okrah aliyesajiliwa kwenye dirisha dogo la usajili akitokea Becham United ya Ghana, alipasua mishipa ya pua baada ya kugongana na mchezaji wa KVZ, katika mchezo wa hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyofanyika Visiwani Zanzibar hivi karibuni.
Okrah ambaye kwenye mchezo wa juzi wa Mashujaa, aliingia akitokea benchi alisema ilikuwa ni ajali mbaya ambayo alitarajia ingemuweka nje kwa kipindi kirefu lakini anashukuru timu ya madaktari na uongozi wa Yanga, walipambana na kumpa huduma bora ya matibabu.
“Nawashukuru sana viongozi na madaktari, hiki walichokifanya ni deni kwangu kuhakikisha naipambania timu kufikia malengo mwishoni mwa msimu,” alisema Okrah.
Kiungo huyo ambaye msimu uliopita aliwatumikia watani zao Simba kabla ya kuachwa mwishoni mwa msimu alisema pamoja na huo kuwa mchezo wake wa kwanza wa ligi kuichezea Yanga, lakini amefurahi kuona timu hiyo ipo kwenye kiwango cha juu chenye uwezo wa kutetea ubingwa msimu huu.
Alisema anatambua Yanga ina wachezaji wengi wenye ubora wa hali ya juu lakini atapambana kutumia kipaji chake na kushirikiana na wenzake ili kufanya vizuri na kuwapa furaha mashabiki zao mwishoni mwa msimu huu.