Na mwandishi wetu
Mshambuliaji mpya wa Simba, Pa Omar Jobe (pichani) amesema kuwa atawanyamazisha kwa kufunga mabao kila atakapopata nafasi ili kuwathibitishia wale ambao hawana imani na kiwango chake.
Jobe ambaye jana Jumatano alicheza mechi ya kwanza akiwa Simba alifunga bao moja kwenye ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Tembo FC kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) FA.
Mchezaji huyo alisema ana kitu cha kuwaonesha mashabiki wa Simba na kwamba hakuwa kwenye kiwango bora kwa sababu ametoka kwenye mapumziko.
“Nikiwa hapa kazi yangu ni kufunga mimi ni mshambuliaji natakiwa kupachika mabao kwa ajili ya klabu ndio maana niko hapa. Watu wana mashaka na mimi kutokana na muonekano wangu lakini hilo si muhimu, nimecheza Ulaya na kufunga mabao 13 msimu uliopita,” alisema Jobe.
“Jana kiwango hakikuwa kizuri, nilipoteza nafasi ya kwanza mpira ulienda nje lakini yote ni mpira wa miguu kama mshambuliaji unapata nafasi unapoteza sio jambo zuri.
“Unajua Simba ni klabu kubwa barani Afrika kabla ya kuja hapa nililijua hili, hata nchini Togo watu wanaizungumzia hata nilipokuja hapa watu wamenipongeza,” alisema Jobe.
Jobe raia wa Gambia ametua Simba hivi karibuni kurithi mikoba ya Jean Baleke aliyerejea TP Mazembe kabla ya kupelekwa Al Ittihad ya Libya kwa mkopo pia.