Barcelona, Hispania
Kocha anayejiandaa kuachana na klabu ya Barcelona, Xavi Hernández amesema kazi yake katika klabu hiyo ilikuwa haithaminiwi na kutahadharisha kuwa itakuwa vigumu kwa kocha ajaye kuifurahia kazi hiyo.
Jumamosi iliyopita, Xavi ambaye ana mkataba na Barca hadi mwaka 2025, alitangaza kuachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu huu, kauli iliyokuja baada ya kupokea kichapo cha mabao 5-3 mbele ya Villarreal.
Msimu uliopita, Xavi aliiwezesha Barca kubeba taji la Ligi Kuu Hispania au La Liga ikimaliza kinara kwa pointi 10 zaidi ingawa msimu huu mambo yanaonekana kuwa magumu, tayari timu hiyo imetolewa kwenye Cope De Rey, Super Copa na kwenye La Liga mambo si mazuri.
“Ni kazi ya kikatili na isiyo na uungwana, inakufanya ujione huna thamani kila siku, Pep (Guardiola) aliwahi kuniambia, niliona pia jinsi Luis Enrique alivyopata shida,” alisema Xavi.
“Tuna tatizo katika yale tunayoyataka, hufurahii, unacheza wakati wote kwa ajili ya maisha yako, ni ukatili, kazi tuliyoifanya haithamiwi kwa kiasi kinachotakiwa, tulikuja hapa mwaka 2021 klabu ikiwa katika moja ya vipindi vigumu zaidi,” alisema Xavi.
Alipoulizwa ni nani hasa ambaye haithamini kazi aliyoifanya, Xavi alijibu kwamba hathaminiwi kwa ujumla.
“Nimekuwa na mtazamo kwamba kila ninachokifanya, sithaminiwi, si suala la kujikuta katika presha, tumetoka katika kipindi kigumu na sidhani kama kazi yetu itatokea ikathaminiwa,” alisema Xavi.
“Wakati wote nimekuwa nikisema kile ninachofikiri, kama nikisema tuna timu ambayo tunaijenga unanishambulia, kama nikisema kwamba hatujawa na Barca ya 2010 pia kunakuwa na shutuma,” alisema Xavi.
Xavi hata hivyo alisema kwamba kwa upande mwingine amejiona ni mtu mwenye kuthaminiwa na rais wa klabu hiyo, Joan Laporta na anamshukuru kwa fursa na imani aliyokuwa akimuonesha.
Akizungumzia mambo ya baadaye ya Barca, Xavi alisema anaamini hata kocha ajaye badala yake katika timu hiyo naye atajikuta akiwa tatizo.
“Ndoto yangu ilikuwa kuwa kocha wa Barca, timu iwe inashinda na kucheza soka zuri, ninajivunia kwa kile nilichoweza kukifanya, ushauri wangu kwa anayekuja badala yangu ni kuhakikisha anafurahia kazi yake lakini hilo haliwezekani,” alisema Xavi.
Pamoja na yote hayo, Xavi ambaye amekuwa na timu ya Barca kwa miaka 17 katika kikosi cha kwanza kabla ya kutimkia Qatar mwaka 2015, amesema hajafunga mlango kuhusu uwezekano wa yeye kurudi Barca kwa mara nyingine.
“Sifuti kabisa uwezekano wa kurudi siku moja, mimi ni mtu wa klabu hii na nipo kwa ajili ya klabu hii pale watakaponihitaji,” alisema Xavi.