Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouf Dabo amesema watautumia mchezo wao dhidi ya Simba kuonesha dhamira yao ya dhati ya kulihitaji taji la Ligi Kuu NBC msimu huu.
Timu hizo zimepangwa kukutana Februari 9 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, huo ukiwa mchezo wa kiporo baada ya ule wa awali kusogezwa mbele.
Kocha huyo raia wa Senegal alisema uimara wa kikosi chake, maboresho waliyoyafanya kwenye dirisha dogo pamoja na muda mrefu wa maandalizi waliopata ndivyo vinavyompa matumaini ya kushinda mchezo huo na kufufua matumaini yao ya kubeba taji hilo msimu huu.
“Kikosi changu kimezidi kuimarika kama ilivyokuwa kabla ya Afcon na kwa sasa tumeongeza ubora kutokana na maingizo mapya, hii inatupa nguvu ya kuifunga Simba na kuthibitisha ubora wetu na dhamira ya kubeba taji la ligi kuu msimu huu,” alisema Dabo.
Kocha huyo alisema anatambua hata wapinzani wao Simba nao kikosi chao kina mabadiliko makubwa kuanzia benchi la ufundi na baadhi ya wachezaji lakini hilo haliwapi presha sababu bado wanahitaji muda kujenga muunganiko tofauti na timu yake ambayo ipo tayari kwa mapambano.
Azam ipo kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 16 ikikusanya pointi 31 katika michezo 13 iliyocheza huku Simba ikiwa nafasi ya tatu kwa pointi 23 katika mechi zai 10.