Na mwandishi wetu
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imekiri kupokea barua ya Simba SC ya kuomba kutumia Uwanja Amaan Complex, Unguja kwa muda hadi Uwanja wa Uhuru na Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam utakapokuwa umekamilika kufanyiwa marekebisho.
Hayo yamesemwa leo Jumanne na Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPLB, Almasi Kasongo na kuongeza kuwa wanaendelea kuichakata barua hiyo na itakapokuwa tayari watawafahamisha Simba na umma wa Watanzania maamuzi gani yamechukuliwa.
“Kwa hiyo niseme tumepokea hiyo barua na tunaendelea kuichakata, itakapokuwa tayari basi tutawafahamisha Simba na umma wa Watanzania juu ya kinachofuata,” alisema.
Hata hivyo, kanuni za Ligi Kuu za mwaka 2023, kanuni ya tisa inayohusu uwanja kwenye kipengele cha nne kinasema wazi timu inayoshiriki ligi kuu itachagua uwanja ndani ya eneo la Tanzania Bara.
“Endapo timu yoyote haina uwanja wa nyumbani unaofaa kwa mchezo wa ligi kuu inaweza kuchagua uwanja mwingine katika mji au mkoa jirani na mkoa wa timu husika ndani ya Tanzania Bara ulio na sifa zinazokubalika na uthibitishwe na kuidhinishwa na TFF, baada ya uteuzi timu haitaruhusiwa kubadilisha uwanja huo kinyume na sababu za kikanuni,” kipengele hicho kinafafanua.
Upande wa pili, Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) limekiri kupokea barua ya maombi ya Simba kuhitaji kutumia uwanja huo katika michezo ya nyumbani ya ligi kuu, Kombe la FA (ASFC) na michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katibu Mkuu wa ZFF, Hussein Vuai alisema: “Nikiri ofisi yangu imepokea barua rasmi kutoka Simba ya Dar es Salaam, kuomba kutumia Uwanja wa New Aman Comlpex katika michezo yake ya nyumbani.
“Kwa heshima kubwa kwa ndugu zetu Simba na tunaona ni jambo linaloweza kuleta faraja kwa mpira wa Zanzibar, endapo litafanikiwa kwa asilimia 100 na kufungua fursa kwa Wazanzibar na Watanzania wanaoishi visiwani humu kuiona Ligi Kuu ya Bara na mashindano mengine ikichezwa Zanzibar.”