Barcelona, Hispania
Kocha wa Arsenal, Mikel Ateta ni miongoni mwa makocha watatu wanaotajwa kuchukua nafasi ya Xavi wa Barca pamoja na Jurgen Klopp wa Liverpool na Julian Nagelsman wa timu ya taifa ya Ujerumani.
Xavi ametangaza hivi karibuni kwamba ataachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu huu wa 2023-24 uamuzi ambao umeacha maswali ya nani atarithi mikoba ya kocha huyo.
Vyanzo mbalimbali vya habari vimemtaja Arteta kwamba huenda akaachana na Arsenal licha ya ukweli kwamba kuna ugumu kwani inaelezwa kuwa kocha huyo amepania kuipaisha Arsenal na haoneshi dalili zozote za kuwa tayari kuondoka katika timu hiyo.
Kwa upande wa Klopp ambaye naye ametangaza kuachana na Liverpool baada ya msimu huu haitoshangaza akienda Barca kwani amenukuliwa akisema kwamba hatoinoa timu nyingine yoyote ya England baada ya kuondoka Liverpool hivyo suala la kwenda Barca si la kulifuta moja kwa moja.

Klopp hata hivyo zipo habari kwamba anasubiriwa kwa hamu kwenye timu ya taifa ya Ujerumani ambako inaaminika mashabiki wengi wanaamini ana uwezo wa kuirejeshea heshima timu hiyo ambayo imekuwa ikipitia kipindi kigumu katika miaka ya karibuni.
Kuhusu Nagelsmann kilicho wazi ni kwamba mara baada ya fainali za Kombe la Ulaya 2024 au Euro 24 zitakazofanyika nchini Ujerumani kuanzia mwezi Juni mwaka huu, kocha huyo ataachana na timu hiyo na hivyo kuwa huru kujiunga na timu nyingine yoyote ikiwamo Barca..