Na mwandishi wetu
Timu ya soka ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars inatarajiwa kurejea nchini Jumatatu hii ikitokea Ivory Coast ilikokuwa inashiriki fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2023).
Katika michuano hiyo, Tanzania iliyokuwa Kundi F na timu za Morocco, DR Congo na Zambia, ilimaliza makundi ikishika nafasi ya mwisho wakiwa na kuvuna pointi mbili.
Katika mechi zake, Stars ilianza kwa kufungwa mabao 3-0 na Morocco kisha ikapata sare ya bao 1-1 dhidi ya Zambia kabla ya matokeo ya suluhu dhidi ya DR Congo.
Akizungumza na GreenSports kwa njia ya mtandao leo Jumamosi, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Cliford Ndimbo (pichani juu), alisema Taifa Stars watarejea Jumatatu na ndege ya Ethiopia.
“Kesho (leo) ndio tunatoka huku tulipo na Ethiopian Airlines na huko (Tanzania) tutafika keshokutwa (kesho),” alisema Ndimbo.
Taifa Stars inatokea katika mji wa Karhogo ambako ilicheza mchezo wa mwisho dhidi ya DR Congo na wachezaji wa timu hiyo wanaocheza nje ya Tanzania, wataondokea hukohuko kwenda katika klabu zao.
Stars ambayo ni timu pekee kutoka Afrika Mashariki katika michuano hiyo, hii ni mara ya tatu kushiriki Afcon baada ya mwaka 1980 nchini Nigeria, 2019 (Misri), msimu huu imefanya vizuri kuliko misimu iliyopita baada ya kuambulia pointi mbili wakati mwaka 1980 iliambulia pointi moja na mwaka 2019 haikupata kitu.