
Na mwandishi wetu
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla ameipa Klabu ya Pamba Jiji Sh milioni 5 ikiwa ni sehemu ya hamasa kwa ajili ya kuikabili Biashara United kwenye Ligi ya Championship.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya utoaji fedha hizo leo Ijumaa katika ofisi yake, Makalla alisema fedha hizo ni kwa ajili ya hamasa ya ushindi wa Pamba kuelekea mchezo huo muhimu.
“Nawaomba muendelee kushirikiana na kupambana ili Pamba ifanye vizuri na hatimaye irejee ligi kuu,” alisema Makalla.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa timu ya Pamba Jiji, Alhaji Majogoro amemshukuru Makalla kwa kuendelea kuisaidia klabu yao kila wakati.
Kwa upande wake nahodha wa timu hiyo, Jerson Tegete alimshukuru Makalla kwa mchango wake kwenye klabu hiyo na kuahidi kupambana kuirejesha timu hiyo kwenye Ligi Kuu NBC.